Ongeza Umakini Sana Kwenye Maamuzi Haya Na Utafanikiwa.
Saturday, May 28, 2022
Tafiti nyingi zinaonyesha binadamu anafanya maamuzi madogo madogo zaidi ya 300 kwa siku moja tu. Maamuzi anayoyafanya ikiwa ni pamoja na ale nini, avae nini, aende wapi, aongee na nani, aamke saa ngapi, afanye biashara gani, ni maamuzi madogo madogo lakini hadi yanafikia zaidi ya 300 kwa siku moja peke yake.
Inaweza ikakushangaza kidogo, lakini ukweli ndio huo hapo kwamba kwa siku unafanya maamuzi zaidi ya 300. Hivyo na kwa sababu hiyo, unatakiwa kujiuliza maamuzi hayo unayofanya ingawa wakati mwingine unaweza usiyaelewe sana ni ya aina gani? yanakusaidia au yanakuharibu? ni muhimu sana kujiuliza swali hilo.
Kwa mfano, kama kila siku unafanya maamuzi ya kula vyakula vya hovyo kama vile vyenye mafuta, kiafya unategemea nini? Au kama kila siku unafanya maamuzi yasiyo ya msingi kwa kutumia pesa zako hovyo unategemea kweli itafika wakati utafikia ule uhuru wa kifedha? Maamuzi mabovu kama hayo ni rahisi tu kukudondosha.
Ukiangalia tokea muda una amka asubuhi hapo ndipo maamuzi yako yanapoanzia, najua utaamua uamke unafuraha au huzuni, au utaamua siku hiyo ufanye kazi kwa bidii sana au kwa ulegevu. Yapo mambo mengi sana ambayo utaamua lakini yote yana matokeo kwenye maisha yetu bila kujali matokeo hayo ni hasi au chanya.
Tambua, ikiwa asilimia 90 ya maamuzi haya madogo madogo unayoyafanya kila siku hayapo sahihi, basi hakuna ubishi lazima ushindwe kwenye maisha. Pia ikiwa maamuzi haya madogo madogo unayoyafanya yapo sahihi kwa asilimia 90, ujue unao uhakika wa mafanikio kabisa na hakuna ubishi.
Kazi kubwa inabaki kwako maamuzi unayoyafanya ni ya aina gani? Ndio maana unatakiwa usikurupuke, kichwa chako kinatakiwa kutulia na kujua maamuzi unayoyafanya yanakupoteza kwenye njia ya mafanikio au yanakuweka kwenye njia halisi ya kufanikiwa kwako.
Kama nilivyotangulia kusema, huwezi kuwa na maamuzi ya hovyo ukategemea kufanikiwa. Mafanikio yako yanategemea sana na maamuzi yako ya kila siku. Kwa lugha nyingine kipimo sahihi cha mafanikio yako ya kesho kinatokana na maamuzi yako ya kila siku unayoyafanya.
Kama kila siku ukiwa makini na maamuzi yako, ni rahisi sana kujua wewe kama kweli utafanikiwa au hautafanikiwa. Ukiongeza umakini kidogo na kujua sawasawa maamuzi unayoyachukua kila siku, basi utaelewa nisemacho hapo, juu ya umuhimu wa kuyaangalia maamuzi yako kila siku.
Mwisho kabisa elewa hivi, kila maamuzi unayoyafanya yana matokeo kwenye maisha yako, eidha matokeo mazuri au mabaya, inategemea tu ni maamuzi gani ambayo umeyafanya. Hivyo kila siku ongeza umakini kwenye maamuzi yako na hakikisha unafanya maamuzi sahihi ili ujenge maisha yako ya mafanikio kwa usahihi pia.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, KIENYEJI ASILIA na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com