Kama Utaruhusu Kelele Hizi…Utashindwa Kufanikiwa.
Friday, May 13, 2022
Usisikilize kila kitu |
Zipo kelele nyingi sana katika dunia hii ya habari. Utasikia hiki mara utasikia kile, ilimradi kukicha tu zipo habari na taarifa nyingi ambazo zinatolewa ambazo lengo lake wewe uzisikie na pengine kuzifanyia kazi.
Usipokuwa makini utajikuta kila kitu unataka kufatilia. Sasa njia ya kuweza kujiokoa na kelele hizo na kuweza kufanikisha malengo yako ni kwa wewe kuweka nguvu zako za uzingativu kwa kile unachokifanya.
Angalia kipi unakifanya, kisha kifatilie kitu hicho kila siku. Kelele za huku mara kule acha kuzifatilia zitakupoteza. Kumbuka, mikwenzi mingi ilimpoteza mbwa mawindoni, usiwe miongoni mwa watu watakao potea kwa sababu ya kelele.
Simamia na fatilia mipango yako kwa kuweka nguvu za uzingativu kwa kile ukifanyacho na utafanikiwa. Kuendelea kusikiliza kelele au kila linalosemwa utakuwa ni sawa na mtu ambaye ameamua kujipoteza yeye mwenyewe.
Katika dunia ya sasa, ni rahisi sana kusikia fursa hii au ile, lakini kwa ukweli uliowazi wewe kama wewe huwezi kufanya kila kitu. Kama ni fursa ni lazima utafanya chache na si kila fursa itakuwa yako.
Hivyo unatakiwa kuwa makini na taarifa unazozipokea. Unatakiwa kuwa mtulivu na usiwe mtu ambaye unaendeshwa na mihemiko isiyo ya maana. Kelele za dunia zisikuyumbishe hata kidogo, fuata malengo yako.
Ikitokea umekubali kuyumbishwa na dunia au na kelele za dunia, basi utaishi kama bendera fuata upepo maana hutafika popote. Utagusa hiki mara kile na kila kitu utakuwa unakianza na kukiacha kila ukisikia kuna kingine kizuri kinalipa.
Kuanzia leo jifunze kuweka masikio yako pamba, jifunze kuweka nguvu zako za uzingativu eneo moja, mahali ambapo utafanya kitu na kitaonekana cha thamani. Ukiziba masikio usisikie kitu, utajenga uwezo mkubwa wa kufanikiwa.
Chukua hatua kwa kufanyia kazi hicho ulichojifunza na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza na kuhamasika zaidi kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com