Kanuni Za Kujua Kusudio La Kuumbwa Kwako.
Tuesday, May 24, 2022
Kila mwanadamu ameumbwa na kusudio lake hapa dunia. Pia itakuwa ni dhambi kubwa kama upo hapa dunia pasipo kutambua hilo kusudio lako. Watu wengi wanashindwa kufanya vizuri katika yale wayafanyayo hii ni kwa sababu watu hao wanafanya vitu ambavyo sio vyao bali ni vya watu wengine.
Watu wengi tunaishi kwa kuigaiga mambo ya watu wengine, yaani utakuta mtu fulani anafanya jambo fulani kisha mtu mwingine naye anaanza kufanya jambo hilo , kitendo hiki ni kujipoteza wewe mwenyewe pasipo wewe kujua.
Hivyo zifuatazo ndizo kanuni za kujua kusudio la kuumbwa kwako;-
1. Muombe mwenyezi Mungu.
Kwa imani uliyonayo basi unashauriwa kutumia imani hiyo hiyo kuomba Mungu akujalie ili uweze kufahamu kusudio lako uwepo wako katika sayari hii. Kwani ukweli ni kwamba Mungu wetu ni mwema na ni muaminifu pia, hivyo tunaamini anatambua kila mmoja wetu lengo lake ni nini hapa duniani.
2. Hakikisha unafanya kitu ambacho unakipenda.
Miongoni mwa mambo ambayo humsaidia mtu ili aweze kujua lengo lake na kuwepo hapa duniani ni pamoja na kufanya mambo ambayo anayapenda.
Wengi wetu tunashindwa kufanikiwa katika maisha hii ni kwa sababu tunafanya vitu tusivyovipenda. Hivyo kila wakati unatakiwa kuhahakisha kila unachokifanya unakipenda kutoka moyoni mwako.
Kama unafanya jambo ambao hulipendi unashauri uachane na jambo hilo mara moja kwani ni sawa na kupoteza muda tu, kwani unatakuwa unafanya ilimradi siku iendee tu.
3. Jitafute/wewe ni nani?
Unashauriwa pia ili uweze kutambua uwezo ulionao ni pamoja na kuwekeza muda mwingi wa kujitafuta wewe ni nani. Ninapozungumzia wewe ni nani hapa ni maana ya kwamba ni lazima uwaze kuwa wewe upo vizuri katika kufanya jambo gani?
Mara baada ya kupata majibu ya kwamba wewe upo vizuri katika jambo gani ndipo unapotakiwa kuwekeza nguvu, muda, akili na pesa katika kulikeleza jambo hilo.
Kama wewe ni mwanamitindo, mfanyabiashara, fundi au jambo lolote lile basi ni vyema ukaweka mkazo wa kiutendaji katika mambo hayo na si vinginevyo.
Pia ni ili uweze kujitambua wewe ni nani zinahitajika akili za ziada za kuweza kujitambua madhaifu na uwezo ulionao katika utendaji wa jambo fulani.
Katika madhaifu uliyonayo basi yafanyie kazi madhaifu hiyo ili weze kuondokana nayo kabisa, ila katika uwezo ulionao basi unatakiwa kuongeza juhudi ili uweze kufanya bora zaidi ya uwezo wako.
Hayo ni baadhi ya ya mambo ya msingi unayopaswa kuzingatia katika kutambua kusudio lako hapa dunia ili uweze kuishi maisha yenye furaha hatimaye kupata mafanikio unayoyataraji.
Ndimi Afisa mipango: Benson Chonya.
bensonchonya23.gmail.com