Mambo Manne Yanayohitajika Katika Mafanikio Ya Mjasiriamali.
Wednesday, May 4, 2022
Safari ya mafanikio kwa mjasiliamali, mara nyingi ni safari ambayo inachangamoto nyingi sana. Kupitia changamoto hizo ndizo huwaangusha wengi na matokeo yake kushindwa kufanikiwa. Ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali kuna mambo ya msingi unayotakiwa kuyajua na kuyafatilia karibu kila siku.
Na ni mambo hayo hayo, ndio yaliyonifanya mimi nishike peni na kalamu ili niweze kukujuza. Nimeamua kufanya hivyo kwa sababu, kama hutayajua mambo hayo, utakuwa ni mtu wa kuanguka anguka sana na kushindwa kufanikiwa. Je, mambo hayo ni yapi, fuatana nami niweze kukujuza moja baada ya jingine.
1. UNG’ANG’ANIZI.
Kuendelea kung’ang’ania na kutaka matokeo unayataka yatokee kwenye maisha yako, naweza kusema hili ni moja ya jambo la muhimu sana katika ujasiriamali. Iko wazi utakutana na changamoto kwenye njia ya mafanikio, lakini huwezi kuchoka ni lazima ung’ang’anie mpaka lile lengo lako liweze kutimia.
Unapokutana na changamoto na ukaamua kuwa mbishi kwa kupambana nazo, hapo utakuwa upo kwenye njia sahihi ya mafanikio yako. Wajasiramali walio wengi ni watu wa kung’ang’ania na kwa sababu hiyo huwasaidia sana kuweza kufikia mafanikio yako. Ukishindwa kuwa king’ang’anizi sahau mafanikio ya ujasiriamali.
2. MAENDELEO.
Lazima uendelee kuwa king’ang’anizi, lakini itakuwa ni kazi bure kama utaendelea kuwa king’ang’anizi na ukashindwa kuona maendeleo kwa kile unachokifanya. Hapa ndipo wajasiariamali wengi ninapoona wanakosea, wanafanya kazi kwa muda mrefu, wiki, miezi, miaka, lakini ukija kuwatamazama wapo pale pale, hili linaumiza.
Lazima uwe wazi kwenye malengo yako ya kijasiriamli. Hiyo ndiyo njia ya mwisho ya kuthibitisha kuwa unafanya progress/maendeleo au unapiga makitaimu. Andika malengo yako ya ujasiriamli na kisha anza kuyatekeleza kidogo kidogo. Kwa kifupi, fanya ufanyavyo, lakini ni muhimu kuona maendeleo ya kile ukifanyacho.
3. MABADILIKO.
Mara nyingi, mabadiliko yanakwenda sambamba na maendeleo. Kama kuna kitu unakifanya na huoni maendeleo yake, ni lazima kufanya mabadiliko kwa kubadili mambo ambayo yanakwamisha usione maendeleo hayo. Kama usipofanya mabadiliko na unaona mambo hayendi unajichelewesha wewe.
Katika hatua hii ya mabadiliko ni kama vile unakuwa unafanya tathmini kwa kuangalia mambo yanaenda au hayaendi. Ukiona mambo hayaendi sawa, kama nilivyokwambia ni ruksa kuweza kufanya mabadiliko, ambayo yatakusaidia kuweza kupata matokeo ambayo unayataka na ya faida kwako.
4. FAIDA.
Hakuna mjasiriamali ambaye anaendesha mambo yake tu kiholela bila kuona faida. Faida ndio lengo la kwanza la mjasiriamali yeyote yule. Unapoona mjasiriamali anang’ang’ania, anafanya mabadiliko na kutaka kuona maendeleo, ujue hapo anachokilenga ni kutafuta faida.
Naamini ukiyapitia mambo hayo manne tena na tena, ni dhahiri utaelewa ni mambo ambayo yatakusaidia sana kuendelea kufanikiwa ukiwa kama mjasiriamali. Huhitaji kukata tama, unachohitaji ni kuendelea kujifunza na kufanyia kazi kila aina ya mafundisho unayoyapata hapa kila siku.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
. DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Whats app; +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com