Kama Unataka Kufanya Mabadiliko Makubwa Katika Maisha Yako, Hakikisha Unasoma Hapa.

Ili tuweze kufanikiwa, kuridhika na kuyafurahia maisha ya mafanikio, wakati mwingine hutulazimu tubadilike. Suala hili la kubadilika lipo kwa ajili yetu, hata kama hatuko tayari kufanya hivyo. Tunaishi katika dunia ambayo inabadilika kila siku. Sasa, iwapo dunia hii iko tayari kubadilika , kwa nini binadamu agome kubadilika kama umuhimu huo upo?

Hata hivyo, tunapokusudia kufanya mabadiliko kwenye maisha yetu, hilo huwa ni jukumu zito na gumu. Kwa mfano pale tunapoamua kubadili mambo fulani, huwa tunaamua kuyaondoa mambo yote ya zamani na kuleta mambo mapya ambayo hatuna uzoefu nayo. Hali hii inaweza ikasababisha tuyumbe, tuogope na hata tukose mwelekeo.

Hata hivyo, tunaweza tukakabiliana na hata kupunguza madhara ya hali hii yenye wasiwasi na mtikisiko iwapo tutajua jinsi ya kukabiliana na mabadiliko haya kwa njia ambazo ni imara kwetu. Haitakuwa rahisi kwetu tena kuyumba na kuanguka kwani hiyo itakuwa na sawa tumejishikiza katika nguzo imara, ambayo sio rahisi kuweza kubomoka.

Ni lazima na muhimu sana kwetu kufanya mabadiliko hata kama wakati mwingine akili na miili yetu huwa inatugomea. Kumbuka, hauwezi kufanikiwa kama hautafanya mabadiliko katika maisha yako, utaendelea kubaki vilevile siku zote. Na kama unataka kufanya mabadiliko haya makubwa katika maisha yako, hakikisha unafanya mambo haya:-

1.Kudhamiria na kujitoa kikamilifu.

Ni muhimu sana kwetu kudhamiria na kujitoa kikamilifu katika kufanya mabadiliko tunayoyahitaji katika maisha yetu. Hata hivyo, kudhamiria na kujitoa huku kunaweza kutudanganya kama hatutaweza kuwa waangalifu kwa kiasi cha kutosha. Hapa namaanisha kwamba, sisi wenyewe tunaweza tukajigawa katika sehemu mbili.

Sehemu moja inakuwa iko tayari kufanya mabadiliko na sehemu inayobaki inakuwa haiko tayari kufanya mabadiliko. Hivyo, kunakuwepo kudhamiria kunakoshindana. Mara nyingi, kudhamiria kunakoshindana husababisha upinzani. Na katika juhudi za kupambana na upinzani huu hatimaye tunajikuta tunakata tamaa na kushindwa kufikia kwenye malengo yetu.

Hali ya kudhamiria kushindana inapokuwepo ndani ya mtu humfanya mhusika aanze kuhujumu juhudi zake binafsi za kukamilisha mabadiliko anayoyataka. Hapa, visingizio na sababu nyingi hutolewa kwa lengo la kuhalalisha kushindwa. Hapa, lawama nyingi kutolewa na watu wengine walioko nje na ambao hawahusiki na mabadiliko tunayotaka kufanya.

Hali hii huhujumu na kuharibu morali au ari ya kufanya mabadiliko. Mara nyingi , siyo rahisi kwa mtu kutambua kwamba, upinzani anaopata unatoka ndani mwake mwenyewe. Vilevile upinzani huu humpeleka mtu kwenye utaratibu mwingine nje ya ule unaohusu mabadiliko anayotaka . Hivyo basi, ni muhimu kudhamiria na kujitoa ili kuushinda upinzani.

 

2.Tunahitaji kuwa na Muundo.

Hili ni suala la muhimu na la msingi katika kuharakisha mabadiliko unayoyataka, lakini mara nyingi suala hili limekuwa halizingatiwi ipasavyo. Muundo ndiyo unaoshikilia na kudhibiti mchakato  mzima wa mabadiliko tunayoyataka kufanya. Unahusu rasimali zote tunazotaka kutumia na mifumo itakayotusaidia wakati tunafanya mabadiliko hayo.

Hivyo, muundo ndiyo  utakaotuhakikishia usalama wetu wakati wa mabadiliko. Unaruhusu tushirikiane na magumu na changamoto zetu na watu wengine, na hivyo kutupunguzia mizigo. Pia unatuhakikishia mafanikio. Kwa maneno mengine nguzo hii ndiyo inayotupatia watu wa kutusaidia na kututia moyo, wa kusherehekea nao tunapofanikiwa, wa kutukumbusha na kutuhamasisha.

Hivyo ni muhimu kwa mtu kuwa na muundo uliothabiti ambao utatoa msaada kwake kwa kiwango kinachotakiwa wakati anapitia kwenye mabadiliko. Ingawa suala la mafanikio ni gumu na linalotisha, lakini linawezekana pia ukiamua. Ikiwa utajiandaa vizuri na kwa ukamilifu, ndivyo utakavyojikuta unarahisisha na kufanikisha safari yako ya mabadiliko.

3. Jambo jingine muhimu ni suala la ufanisi.

Kuwa na ufanisi binafsi utakaokuwezesha kusonga mbele ni kitu muhimu sana kwako. Hapa tukiwa na maana kuwa wakati mwingine suala zima la ujuzi au uzoefu huwa unahitajika katika kuleta mabadiliko unayoyataka. Pia kuwa na muda, nishati na uwezo unaohitajika kwa ajili ya kujifunza na kujipatia maarifa na ujuzi.

Kumbuka kama dunia inabadilika kwa nini wewe usibadilike? Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya mabadiliko katika maisha yako kwa kufanya mambo hayo.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea mtandao huu wa kwa kujifunza vitu muhimu vitakavyobadili maisha yako.

TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.

IMANI NGWANGWALU



Iklan Atas Artikel

Iklan Tengah Artikel 1

Iklan Tengah Artikel 2

Iklan Bawah Artikel