Jambo Hili Lisiwe Kizuizi Cha Mafanikio Yako...Kila Mtu Anapitia.
Tuesday, May 17, 2022
Haijalishi unafanya kitu gani na una uhakika gani wa kukamilisha kitu hicho, lakini huwezi kukipata kitu hicho moja kwa moja kwa jinsi unavyotaka wewe iwe. Yapo mambo ambayo ni lazima yataingilia malengo yako hayo kwa namna moja au nyingine.
Unapojiwekea malengo, utafika wakati malengo yako yataingiliwa tu. Itafika wakati pesa ambayo ulikuwa umeitenga kwa ajili ya malengo fulani, unaweza ukashangaa umeitumia kwa dharura na kujikuta tena unaanza upya.
Lakini pia unaweza ukawa umeamua kufanya kazi fulani inayohitaji utulivu, lakini ukashangaa simu ikaita, au ukapokea dharura ya kuitwa pengine na bosi wako na miingiliano mingi kama hiyo ambayo naweza kusema haikwepiki kirahisi.
Yanapotokea mambo kama haya ambayo yanaingilia ndoto na malengo yako isifike mahali ukajikuta unakata tamaa. Unachotakiwa kuelewa ni kwamba, mwingiliano wa vitu katika malengo, ni kitu ambacho kinamtokea kila mtu na kwa wakati wake.
Mwingiliano wa mambo ukizidi, ni sumu ya mafanikio yako. |
Kama ikitokea umepoteza mwelekeo na huoni tena dalili ya kufanikiwa kutokana na mambo mengi kuingilia ndoto zako, usikate tamaa, unatakiwa kurudi haraka sana na kuendelea kuifatilia ndoto yako.
Usipoteze muda wako kulalamika au kulaumu hali ambayo imekupata, badala yake tumia muda huo, kutafuta njia ambayo itakufanya uirudie ndoto yako haraka sana na sio kuipotezea kama ambavyo unataka kufanya.
Ni kawaida sana kwa mambo ambayo yanaonekana kwa hombre ya kawaida hayawezekani, kuingiliwa na vitu ambavyo hukutarajia. Lakini ukikata tamaa na kusema ndio basi, uwe na uhakika utaipoteza ndoto yako.
Weka mkazo katika akili yako wa kusahau karibu kila kitu nakuamini, unaweza kuirudia ndoto yako hadi kuifanikisha, hata kama hapa kumetokea mwingiliano mkubwa sana ambao kwa uwazi umeonekana kukuvuruga na kukuchanganya kabisa.
Kuingiliana mambo ambayo hukutegemea kunapokuja kama huelewi vizuri, unaweza ukaacha kila kitu, lakini nikwambie hivi tu, kitu hiki kidogo kisiwe kizuizi kwako cha kukuzuia kufanikiwa hata kidogo.
Maisha ya mafanikio makubwa bado yanakuja kwenye maisha yako, changamoto ndogo kama hizi kwako kutokea, anza kuzichukulia kama fundisho la kukukomaza na kukupeleka kwenye mafanikio makubwa. Jipe moyo na inawezekana.
Tunakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio yako makubwa.
Daima tupo pamoja mpaka maisha yako yaimarike na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza kila siku maisha na mafanikio.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com