Ikiwa Unaishi Hivi, Maisha Yako Ni Mafupi Sana.

Ni jambo ambalo watu hulisema  mara nyingi bila kujua maana yake. Unaweza kukuta mtu akisema, ‘ndio maana amekauka, ana roho mbaya sana’. Ukimuuliza ni kwa nini anahusisha kukauka au afya mbaya na roho mbaya au kukosa upendo alikonako mtu, hataweza kukupa jibu sahihi. Lakini, anajua kwamba, kukauka huwapata wenye roho mbaya. Kauli hiyo ina ukweli mkubwa wa kutosha. Watu wengi ambao wanatengeneza nguvu nyingi hasi, hatimaye nguvu hizo huwarudia na kuwadhuru.

Kwa sehemu kubwa, madhara ya nguvu  hizo huja kujitokeza kwenye miili yao. Mtu ambaye anaumwa mara kwa mara, anaweza kuwa anaumwa tu kwa sababu nyingine, lakini pia anaweza kuwa anaumwa kutokana na nguvu hasi anazotengeneza. Nikisema nguvu hasi, nina maana ya kufikiri na matendo ambayo yanamuumiza mwenye mawazo na matendo hayo, pia wale wanaomzunguka. Kwa mfano, mtu asiyeweza kusamehe, mwenye visasi, mwenye kijicho, mpenda makuu, mshindani na mengine ya aina hiyo.

 Kuna watu ambao hutengeneza sana nguvu hasi kwa kufikiri kwao na tabia zao. Kwa kawaida, nguvu hasi huwa zinadhuru hisia na mwili wa mhusika. Kwa vipi? Hebu tutazame kushindwa kusamehe na kijicho. Mtu ambaye hawezi kusamehe, anajiweka mahali ambapo muda wote anakuwa kwenye hasira, hisia chungu na mikakati ya kulipa kisasi. Hii ni sawa na mtu ambaye ana kijicho, kwa mfano. Huyu naye, muda mwingi wa maisha yake, atakuwa akiumia kwani, kila wengine wakifanikiwa kwa chochote, atajihisi vibaya tu. kwa hiyo, hisia zake zitakuwa zinachokozeka karibu muda wote.

Kwa kawaida, hisia zetu zinapochokozeka, tunaiiingiza miili yetu kwenye kuzalisha kemikali au homoni ambazo wakati huo hazihitajiwi. Kwa uzalishwaji huo wa kemikali zisizohitajika mwilini, tunaiumiza miili yetu kwa njia mbalimbali. Kemikali hizo, hatimaye huanza kutuumiza kwa kuteleta maradhi mvalimbali miilini mwetu. Hili ni jamba ambalo limethibitishwa kitaalamu.


Kuna maradhi zaidi ya kumi ambayo chanzo chake ni mihemko yetu, maradhi ambayo kitaalamu hufahamika kama Emotionally Induced Diseases. Haya ni pamoja na maumivu ya mwili, tumbo, kufunga choo na mengine. Ndiyo maana, wale watu wote wanaokwenda hospitalini wakiwa wanaumwa, ambao wanaambiwa vipimo havioneshi maradhi yoyote, ukiwachunguza, utagundua kwamba, wanakabiliwa na hofu, mashaka, visasi  na matatizo mengine ya kihisia.

Sisemi kwamba, wote wanaopimwa na kuonekana hawana maradhi ndivyo walivyo, hapana. Lakini wengi kati yao ndivyo walivyo. Hata wale wanaodaiwa kuwa na mapepo pia, utakuta baadhi ni wale wenye hisia chungu. Kwa sababu ya maumivu ya kimwili na yale ya kiakili, unakuta watu hawa wakiwa dhaifu. Kama walivyo wagonjwa wengine, suala la udhaifu wa kimwili hujitokeza sana kwa watu hawa, kwani pamoja na maradhi yanayoletwa na hisia chafu, kinga ya mwili hushuka sana pale miili inapohemkwa mara kwa mara.

Ni rahisi kwa hali hiyo, watu wenye roho mbaya kukauka au kukosa afya imara. Ingawa siyo kweli hata hivyo kuwa watu wote wenye afya mbovu, inatokana na roho mbaya, hapana. Lakini, kwa wale walio na roho mbaya, yaani kufikiri na tabia zenye kuzalisha nguvu hasi, ni rahisi zaidi kwao kukosa afya bora kama tulivyoona. Ndiyo maana tunasema hivi, kama unaishi maisha haya kuwa na roho mbaya tu, maisha yako ni mafupi kwa sababu utakuwa ni wa afya mbovu kitu ambacho ni hatari sana kwako.

Nakutakia kheri ya mwaka mpya, endelea kutembelea kujifunza na kuhamasika kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,




Iklan Atas Artikel

Iklan Tengah Artikel 1

Iklan Tengah Artikel 2

Iklan Bawah Artikel