Hawa Ndio Watu Hatari Usiowajua, Wanaonyonya Nguvu Za Wengine.

Inaweza kuonekana kama ni kitu cha kushangaza lakini huu ndio ukweli wapo watu wanaonyonya nguvu za watu. Watu hawa wana uwezo wa kumwandama mtu hadi anakufa bila kujua. Watu hawa hawajafa,wako hai na tunaishi nao, wengine wakiwa ni watu wetu wa karibu sana, kama wazazi, wapenzi, watoto, jirani, marafiki au mabosi wetu. Hufanya vipi kunyonya nguvu zetu? Hutumia njia za aina mbalimbali, ambazo huzaa matunda kweli.

Mtu anaweza kuuliza, inawezekana vipi mwingine anyonye nguvu zangu na hizo nguvu ni zipi? Kwa mfano, mimi ninapo kuwa nakukera kila siku, ninakugusa kihisia. Ninapokugusa kihisia, unaumia kihisia na kimwili. Baada ya muda Fulani wa kero zangu, nakuwa nimekupa athari kubwa kimwili na kiakili bila mwenyewe kujua na kama imeshawahi kukutokea umekerwa na mtu huwa inapelekea hata unapokutana na mtu huyu anayekukera unakuwa unajisikia vibaya.

Hebu pia tuchukue mfano wa bosi na mtumishi wake. Kama bosi ni mtu wa maringo, dharau, kulaumu bila kujali nini kimefanyika, mkandamizaji na asiyejali kuhusu madhila ya wengine, ni wazi aliye chini  yake ataumia tu, kwanza, kihisia, halafu kimwili. Ataichukia kazi yake na hatimaye anaweza kufika mahali akaona maisha haya maana aliyoitarajia.

Ni vigumu kubaini mtu ambaye ni mnyonya nguvu mapema, lakini kwa kuelekezwa, mtu anaweza kuwa makini na kuwabaini watu wa aina hiyo popote walipo au watakapokuwa. Nimeamua nikuelekeze au kukutajia sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine na kuwaacha wakiwa maganda matupu, huku wakiwaacha wakiwa wanyonge hawajui ni kipi cha kufanya.

Hizi ndizo sifa za watu wanaoweza kuwanyonya wengine:-

1. Kuna watu ambao tunanaweza kuwaita, “miye maskini.”

Hawa ni watu ambao muda wote unapokutana nao, wanalalamika tu. Hakuna siku ambayo utakutana nao ukute wanazungumzia mambo mazuri au wanafurahia hali. Kila siku wao ni walalamikaji, wanaoamini kwamba, wanaonewa na kuteswa. Unaweza kukuta ni watu wa kulalamika au kukosoa tu, lakini bila kutoa pendekezo au kuonesha ni  njia zipi zingepaswa kufuatwa au njia zipi zingetatua tatizo.

Wao wanaona kwamba, wanaonewa, wananyimwa nafasi, wanatafutwa na kuchukiwa. Hawa kwa kawaida hawana uwezo wa kusema lao, kusema wanachofikiria au walichobuni, hapana. Hata kama wanatakiwa kusema kuhusu jambo fulani maalumu, ambalo halihusiani na kuonewa na mtu, watajikuta wakiingia kwenye kulaumu au kukosoa kwanza, ndipo waweze kujibu, kama basi watakuwa na uwezo wa kujibu.

Hawa ni wanyonya nguvu za wengine. Hawa ni watu wa kuepukwa sana. Kama mtu wa aina hii anakujia na kutaka mjadili jambo, ambapo anaanza malalamiko au kukosoa kwake, huna budi kutafuta sababu ya kukataa kuwa karibu naye. Ni lazima ufanye hivyo, kwani akikuzoea ni lazima atakunyonya nguvu zako zote.


2. Kuna watu ambao wao ni wakuzaji wa mambo.

Hawa ni wanyonya nguvu pia ambao wao kitu au jambo dogo hufanywa kubwa hadi mtu anaweza kuamini kwamba ni jambo kubwa kweli, ingawa awali alijua ni jambo dogo. Hawa wako maofisini na majumbani. Mtu anaumwa na mafua, lakini atalalamika, atagumia na kuaga kabisa na kuacha kabisa wosia, kwamba anakufa.

Yeye mwenyewe huyu anayefanya visa hivyo anaamini kwamba, kwa kufanya hivyo, atapata huruma zaidi, ataona watu wanavyohangaika kuonesha wanavyomjali na kutaka kupima umuhimu wake. Kwa kawaida kukuza kwao mambo kunaweza hata kusababisha hata wengine wakaugua zaidi au hata kupoteza maisha kabisa, kutokana na kuongeza chumvi sana kwenye maneno yao.

3. Kuna wale ambao kwa lugha ya mtaani tunawaita wameza kaseti

Hawa ni wale ambao wanataka waongee wao tu, wanataka wao ndiyo wasikilizwe  na mwingine anapotaka hata kusema moja hapewi nafasi. Mtu atazungumza yeye kuanzia mwanzo hadi mwisho, hata kama ni kwa saa tatu mfululizo. Mwingine anapotaka kuongea, yeye ameshamkatisha na kuzungumza yeye. Hataki kuona mtu mwigine akizungumza kama yeye yupo. Hata kama ni mgeni mahali, akishapewa nafasi ya kuzungumza, huzungumza kweli.

Hajali kama kuna mtu ambaye anataka aseme hisia zake, hapana. Inafika mahali, kama unamsikiliza unachoka kabisa. Hatajali, hata kama utamwonesha kutokujali. Kama ni nyumbani au ofisini, hatajali kukupotezea muda wako kwa vyovyote vile. Kama ni ushauri aliomba kwako, yeye ndiye atakupa ushauri kwa sababu, hatakupa nafasi ya kuzungumza katika kumshauri. Hawa ni wanyonya nguvu ambao tunao kila siku.

4. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuwafanya wengine washitakiwe na dhamira.

Kila wakati linapotoea jambo , juhudi yao kubwa ipo kwenye kutafuta njia ya kulaumu ili wengine washitakiwe na dhamira. Wakati mwingine jambo liko wazi kabisa kwamba, hao anaowalaumu hawahusiki, lakini ni lazima atalaumu tu. Hata kama atafafanuliwa na kuona kwamba, anaowalaumu hawana tatizo, bado atasema, ‘hata kama hamtaki anahusika kidogo’Wanyonya nguvu hawa wanatafuta kasoro ili walaumu, ili mtu mwingine ajisikie kukosa, ashitakiwe na dhamira.

Anaweza kuangalia mtu anavyofanya kazi Fulani na kuona ni nzuri sana. Lakini atajaribu kwa kadiri awezavyo kumkosoa mtu huyo kwa kitu ambacho wala wakati mwingine hakihusiani moja kwa moja na kazi ile. Anaweza kusema ‘ile kazi ya mwaka jana angefanya hivi tusingekosa tenda’ lengo ni kumfanya mtu ashitakiwe na dhamira. Hataki kusifia hii kazi nzuri ya sasa, anataka kukosoa ya zamani ambayo iliharibika.Dawa ya hawa ni kuwapuuzia.

5. Kuna wanyonya nguvu wengine ambao ni wale wasioisha kuwa na matatizo yanayohitaji ushauri.

Asubuhi atakuja kukuomba ushauri unaohusu jambo Fulani, mchana atakuja na jioni atakutafuta. Wakati mwingine ushauri anaoomba ni wa kawaida tu. Ni vizuri kumwonesha kwamba, unajali anachosema, lakini ni vema kila wakati kumwonesha kwamba, huna jibu, siyo huna nia ya kumsaidia kwenye tatizo lake. Ajue kwamba, huna jibu kwa sababu hujui. Ukikosa njia au jibu mara kadhaa, atakata tamaa na kukuacha. Usimwoneshe jeuri au dharau ama kisirani.

6. Kuna wanyonya nguvu ambao kazi yao ni kuudhi kwa maneno ya kushushua na kushushua.

Badala ya kunyamaza, akikuona na nguo ya aina Fulani, atakwambia, ‘bwana mzee huwezi kuvaa nguo za mtumba kwa hadhi yako vipi’ Ni wakati ambao kila mkikutana , watatafuta namna ya kukera kihisia zako na kujaribu kukushushua. Anaweza mtu kusema ‘ mbona afya yako inazidi kuwa mbaya’ bila hata sababu ya msingi. Ni watu ambao muda wote wanataka kuumiza hisia za mwingine.

Bila shaka umeshawahi kukutana na mmoja kati ya wanyonya nguvu hawa. Jitahidi wakati wote kuwa makini wasije wakafanikiwa kukuweka chini ya himaya zao. Jitahidi kuwabaini na kujua namna ya kuwaondolea mbali kwenye maisha yako.

Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea kwa kujifunza zaidi na kuhamasika.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,







                                                           

Iklan Atas Artikel

Iklan Tengah Artikel 1

Iklan Tengah Artikel 2

Iklan Bawah Artikel