Ukilenga Kutafuta Pesa Ya Kula Utapata Lakini…
Sunday, June 5, 2022
Kila mmoja anajitahidi kutafuta pesa popote anakojua. Habari njema ni kwamba kila anayetafuta pesa hii ya KULA anapata. Lakini..
Wengi wa wale wanaolalamika kupata pesa kidogo ni wale walioweka malengo ya kutafuta pesa ya KULA. Ukiweka malengo ya KULA, ujue malengo hayo ni madogo sana na kwa vyovyote vile yatavutia pesa kidogo sana kwako. Mtu yeyote mwenye malengo ya kupata pesa ya KULA, hawezi kuweka utajiri kama kipaumbele chake. Na mwisho wake ujikuta hana ndoto yoyote ya kutajirika maisha yake yote.
pamoja na kuipata, wengi wamekuwa wakilalamika kuwa ni ndogo na kwamba inatosha kula tu! Wengi wanatamani kupata pesa nyingi zaidi ya hiyo wanayoipata kwasasa. Kwaujumla, wengi wanashangaa ni kwanini hawapati pesa ya kutosha kuweza kufanya mambo makubwa zaidi ya KULA na kulipa ADA za watoto.
Sababu mojawapo ya kushindwa kupata pesa ya kutosha ni malengo mahususi tunayojiwekea kabla ya kutafuta pesa. Watu wengi wakiamka asubuhi, malengo yao makubwa kabisa ni kutafuta pesa ya KULA, ADA na kujenga NYUMBA ya makazi. Wengine akijikakamua kidogo analenga kununua GARI la kutembelea. Malengo ya watu yanabainishwa kwenye maongezi yao ya kawaida. Pindi ukiwasikiliza watu, utasikia wakiambizana kuwa “mimi natafuta pesa ya kula basi! Wengine utawasikia wakisema “natafuta pesa kwaajili ya watoto”wengine wamekwenda mbali na kusema kuwa wanatafuta pesa, “ili watoto wao angalau waweze kwenda choo” Ni wazi kuwa maongezi ya namna hii, yanakupa jibu la moja kwa moja kuwa watu wengi wana malengo ya kutafuta kiasi kinachotosha KULA, kulipa KARO na kujenga NYUMBA ya makazi basi! kwamba zaidi ya hapo ni bahati tu.
Ukweli ni kwamba, pesa ya KULA siku zote huwa ni ndogo japokuwa inapatikana kila ikitafutwa. Pamoja na kupatikana kila siku, tatizo lake ni moja; kwamba, ikishapatikana muhusika anakuwa tayari ana njaa na hivyo kuitumia mara moja. Ikishaisha muhusika uenda kutafuta tena, na huo ndio unakuwa mzunguko na mtindo mzima wa maisha ya kila siku.
Kujiwekea malengo ya kutafuta pesa ya KULA na ADA siyo jambo baya! Ubaya unakuja pale utakapofanya suala la kutafuta pesa ya KULA kama lengo lako kuu. Mara nyingi watu waliofanikiwa wanatushauri kuyaweka malengo ya KULA na ADA ndani ya malengo makubwa zaidi (Utajiri). Tunahimizwa kuachana na utamaduni wa kuweka KULA na ADA kama malengo makuu katika maisha, kwasababu, kwa kufanya hivyo tutazidi kupoteza muda mwingi na matokeo yake hututakaa tupate muda wa kufanya mambo makubwa.
Kwa mfano: “Ikiwa wewe unaishi DAR-ES-SALAAM na lengo lako kuu ni kwenda KARAGWE, maana yake, inabidi ujipange kutafuta jinsi ya kupata pesa itakayokuwezesha kufika KARAGWE. Pesa ya kufika KARAGWE ikishapatikana, maana yake ni kwamba sehemu zote za njiani kabla ya kufika mwisho wa safari yako kwa vyovyote vile, utafika sehemu zote za njiani japo hilo halikuwa lengo lako kuu. Sehemu za njiani ambazo kwa vyovyote vile lazima upite ni pamoja na Morogoro, Dodoma, singida, Tabora, Kahama n.k. Sehemu zote hizi utaweza kufika kwa kutumia nauli ile ile ya DAR-ES-SALAAM hadi KARAGWE”
Mfano huo hapo juu, unatufundisha kwamba tunahitaji kuweka juhudi na maarifa yetu kwenye vitu vikubwa kama vile miradi ya maendeleo (majumba ya kupangisha, kilimo biashara, viwanda, biashara kubwa n.k). Tukiwekeza akiri zetu kwenye mambo kama hayo ni wazi kwamba pesa ya KULA na ADA za watoto zitapatikana humos humo ndani ya miradi hiyo. Kitu cha msingi hapa ni kuhakikisha tunajizuia kufanya kazi ya kutafuta pesa ya KULA na ADA kama malengo yetu makuu. Tusifanye KULA na ADA kuwa mwisho wa safari yetu BALI suala la pesa ya kula na ADA liwe ni sehemu za njiani kuelekea Kwenye ndoto kubwa (Utajiri).
Wito wangu kwako msomaji ni wewe kuiambia akili yako na nafsi yako mwisho wa safari yako, yaani safari ya kuelekea kwenye maisha unayotamani kuishi. Naamini ukiweza kuiambia ukweli akili na nafsi yako, basi ujue hapo utakuwa umefikia hatua ya kutafuta pesa nyingi zaidi ya hiyo ya KULA na kulipa ADA. Ili linawezekana, limewezekana kwangu, limewezekana kwa wengine na hakuna sababu yoyote ya kutowezekana kwako.
Endelea kukuza uelewa wako juu ya namna ya kupata pesa zaidi ya ile ya KULA na kulipa ADA za watoto. Fanya hiyo kila mara kwa kutembelea mtandao wako wa .