Tabia Za Kiutendaji Zinazowatofautisha Matajiri Na Maskini.
Thursday, June 16, 2022
Leo nitazungumza na wewe kuhusu tabia kuu ambazo huwatofautisha watu waliofanikiwa na wale wasiofanikiwa, hivyo naomba ukae mkao wa kula kwani chakula hiki ni adimu sana pia ni maalum sana kwako wewe msakatonge mwenzangu.
Sababu kubwa ya watu wengi waliofanikiwa na ambao wanaishi ndani ya ndoto zao ni kwamba watu huamini sana kile ambacho wanakifanya. Kuamini kile wanachokifanya ndicho kilichowapelekea watu hao waendelee kuishi ndoto zao kila jua lichomazapo.
Sababu nyingine ambayo inawafanya watu wenye mafanikio waendelee kufanikiwa ni kwamba watu hao mara baada ya kuona changamoto fulani wao walitafuta njia ya kutafuta majibu ya changamoto husika.
Hiyo ni kwa upande waliofanikiwa, ila unapokuja upande huu mwingine ni kwamba watu wengi wameshindwa kuziishi ndota zao kwasababu, mosi ni kwamba watu hao huwa hawamini kile ambacho wanakifanya.
Hivi hujawahi kukutana na mtu fulani kisha akakwambia nafanya jambo hili kwa kujaribu tu? Bila shaka utawakuta umeshawahi kukutana na watu wengi wenye kauli kama hizi. Ukichunguza kauli kama hizi utagundua bayana ya kwamba ni wazi kabisa watu hawa hata kile wanachokifanya hawakiamini, kwa mtindo huu mafanikio yapo kweli?
Pamoja na kutoamini kile wanachofanya lakini pia watu hawa ni wazuri sana wakutafuta sababu, na sababu hizi ni zile zisizokuwa na msingi yaani watu hawa ni wazuri sana kwa kutafuta visingizio.
Ukimuuliza hivi kwani hujafanya hivi? Mtu huyo atakuja na majibu ya kwa sababu ya.........., majibu ya kwa sababu mara nyingi katika safari ya mafanikio huwa si ya majibu ya msingi bali huwa ni majibu ya kujikatiza tamaa tu.
Hivyo ndugu yangu kama ni kweli unataka mafanikio ya kweli unatakiwa kufahamu ya kwamba kama kweli umeamua kufanya jambo fulani wewe fanya ila kama hauhitaji mafanikio basi endelea kutafuta sababu za kutofanya.
Mpaka kufikia nukta hiyo sina la ziada nikutakie siku njema na mafanikio mema.
Ndimi: Afisa Mipango Benson Chonya.