Ni Muhimu Kutambua Mafanikio Ni Utamaduni.

Utamaduni ni kigezo cha msingi kwa maendeleo ya jamii yoyote. Hakuna taifa lilowahi kuendelea bila kujali utamaduni, kutii, na kufuata misingi muhimu ya utamaduni wao.
Nchini kwetu vitabu vingi vimeeleza maana ya utamaduni kwa ama upotoshaji mkubwa au tafsiri nyonge, kwa mfano, vitabu vingi vinaufafanua utamaduni kama ngoma, harusi, mavazi, vyakula, lugha, nyimbo, mila na desturi.
Kweli hivi vinaweza kuwa viashiria au vipengele vya utamaduni, lakini ni kweli utamaduni ndiyo huo? Matokeo ya tafsiri hizi na dhalimu ni kwamba watoto wetu wanakuwa na kuelewa kuwa utamaduni ni ngoma au nyimbo, kuvaa manyoya, kucheza na nguo zilizochanika mbele ya viongozi uwanja wa ndege kwa lengo la kuwaburudisha wazungu wanaokuja kutembelea nchi yetu. Huo ni udhaifu mkubwa wa mitaala yetu.
Kimsingi utamaduni unatafsiriwa katika nyanja kuu tano;
Moja, ni fikra na namna mtu anavyofikiri. Eneo hili ndilo limekamata sehemu kubwa ya matendo ya utamaduni wa mtu na matendo yake ya kila siku.
Pili, mitazamo, ni eneo muhimu la utamaduni. Hapa akili imekamatwa na desturi zilizozaa mitazamo inayomuongoza mtu kufanya anachotaka  na kuamini anachokiamini.
Tatu, mielekeo/utashi wa kimaisha, nalo ni sehemu ya utamaduni wa jamii yoyote ile. Kila mtu ana mwelekeo anaouweka katika kupambana na maisha ili kufikia maendeleo yake na familia. Mielekeo ndiyo inayomtengeneza mtu kuwa mnyonyaji au mzalishaji.
Nne, imani, Yaani kile mtu anachiokiamini na kukiishi ni kigezo muhimu cha kumfanya yeye aendelee au abaki maskini. Imani ya mtu husanifu mitazamo na uamuzi wa kimaisha.
Tano, mila, jadi na desturi. Hizi zinajenga mtu na kumuumba respeto alivyo. Na mara nyingi hujenga kanuni au taratibu za kuishi. Mila jadi na tamaduni ndizo huunda michepuo ya akili ya watu. Binadamu anaijua dunia kwanza kupitia jadi, mila na desturi ambayo ni kanuni za msingi za kujenga ufahamu kwenye akili ya mtu. Ndiyo maana mila desturi na jadi hazijaandikwa popote.

Haya ni mambo ya muhimu katika utamaduni wa jamii yoyote ulimwenguni. Kuyadharau na kukimbilia ngoma, nyimbo na mavazi ya asili ni sehemu ndogo ya ukweli wa nini maana ya utamaduni.
Tukifahamu hivyo tunaweza kuweka sera na mikakati ya maendeleo kwa kuzingatia utamaduni wa jamii husika. Na ikumbukwe kwamba hakuna jamii hata moja duniani yenye utamaduni mbaya. Kila linalofanyika ndani ya jamii linasababu yake, hata kama ni mbaya kwa mwingine.
Kwa Waarabu nguruwe ni haramu, lakini kwa Wazungu nguruwe ni nyama nono; Utamaduni kwa Waafrika nyoka ni adui mkubwa lakini kwa Wachina nyoka ni nyama nono! Hakuna utamaduni mbaya hapa duniani bali kuna desturi na vitendo vibaya ndani ya jamii fulani.
Pili, utamaduni hauna madaraja, kwamba, utamaduni wa jamii fulani ni mzuri kuliko utamaduni wa jamii nyingine. Wengi wamepotoka na kuvurugwa na utamaduni wa kizungu ulioletwa na wakoloni. Wanajaribu kudharau tamaduni zao na kujaribu kuishi uzungu ambao wengi umewapeleka kuzimu na kuvuruga akili zao, sasa wamegeuka kuwa watumwa wa wazungu. Michepuo ya akili hujengwa na tamaduni asili siyo za kigeni. Ndiyo maana tunasoma lakini hatuna wabunifu wala wavumbuzi.
Utamaduni unabeba vipengele vya msingi vya mchakato wa maendeleo na unasaidia kuimarisha kujitegemea, mamlaka ya kujiamlia mambo yako mwenyewe na ni kitambulisho cha taifa na ndiyo maana ni muhimu kutambua mafanikio ni utamaduni pia.
Bila kutii na kuchambua fursa na vikwazo vya utamaduni wa jamii unayotaka kuiendeleza, kamwe huwezi kupata maendeleo. Hii ni sababu inayofanya maelfu ya miradi ya Benki ya dunia kushindwa kuleta maendeleo yoyote katika nchi maskini ni kutotii utamaduni wa jamii husika.
Mathalani mwananchi wa Uingereza anachofikiria kwanza akipata fedha ni tofauti na mwananchi wa China na hata Vietnam. Vivyo hivyo, ukimpa laki moja Mchaga wa Moshi, na Mnyiramba wa Singida kiasi hichohicho na uwaulize wanataka kufanya nini, fikra na mipango inatofautiana pia.
Ukitumia mabilioni ya fedha kununua chakula na vijiko vya misaada kuwapelekea waathirika wa Tsunami huko India kaskazini na Bangladeshi, itakuwa ni upotezaji wa fedha. Maana utamaduni wa Wahindi ni kula kwa mkono, hawatatumia vijiko kamwe.
Hii ni mifano michache ya kuonyesha jinsi gani utamaduni una nguvu katika kuchochea na kuzuia maendeleo. Miradi yoyote ya maendeleo duniani inabidi itanguliwe na uchambuzi wa utamaduni wa mahali husika ili kuona fursa na vikwazo vilivyomo kwenye utamaduni huo. Vinginevvyo ni kupoteza fedha na muda bure.
Miradi ya maendeleo ni lazima iweze kutokana na jamii yenyewe. Ndiyo maana ni muhimu jamii ichague vipaumbele vya maendeleo, kwani yenyewe ikachagua itaakisi utamaduni na mahitaji yake, na kuifanya ishiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wake.
Yapo hata mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yalifanya juhudi kubwa za kuanzisha miradi ya maendeleo vijijini bila kuzingatia utamaduni wa mahali hapo. Miradi mingi imeishia kupoteza fedha na muda. Umaskini umebaki palepale. Mradi unaobuniwa Ulaya na wazungu, ukaletwa kijijini Chabutwa, kamwe hauwezi kuzaa matunda wala kudumu.
Unaweza kukua kwa siku za mwanzo lakini hauwezi kuondoa umaskini wala kuwa endelevu. Lakini mradi utakaobuniwa na wanakijiji wa Chabutwa wenyewe, ukapata msaada wa mashirika au serikali huo utakuwa endelevu na utaleta mafanikio makubwa na ya kudumu kwa wanakijiji. Hii ni kwa sababu utakuwa umetoka kwao na umezingatia utamaduni wao.
Wanafunzi na jamii kwa ujumla wanapaswa kufundishwa ukweli kuwa kile ambacho utamadani unagusa cha kwanza kabisa ni fikra, mitazamo, miiko, mwelekeo na wala siyo ngoma na nyimbo tu kama ilivyozoeleka.
Lazima wafundishwe mambo mazuri katika utamaduni wetu na yale mabaya ili wajue namna ya kuyaepuka mabaya na kuyaendeleza mazuri.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA MTEMI ZOMBWE, DAR ES SALAAM.

MAWASILIANO- 0713 000027

Iklan Atas Artikel

Iklan Tengah Artikel 1

Iklan Tengah Artikel 2

Iklan Bawah Artikel