Hii Ndiyo Silaha Kubwa Ya Mjasiriamali Katika Kufikia Mafanikio Makubwa.
Sunday, December 19, 2021
Wahenga walisema: “Maisha ni kuona mbele.” Huu ni usemi unaompa mjasiriamali matumaini ya kusonga mbele pasipo kutumia muda mwingi kuwaza yale aliyokwishafanya.
Katika maisha ya kila siku kwenye ujasiriamali, wajasiriamali wanakumbana na changamoto nyingi. Changamoto hizi wakati mwingine huwasaidia kuona mbele na hatimaye kuwa watu wenye mafanikio.
Kwa mfano, kama mtu anajishughulisha na ujasiriamali halafu akawa anasumbuliwa na mamlaka zinazohusika na urasimishaji wa biashara kwa sababu za kutorasimisha shughuli zake, akiamua kurasimisha biashara yake atafanya shughuli zake bila kubughudhiwa.
Mwisho wa siku atakua kibiashara, hivyo kuchangia maendeleo ya nchi yake kwa kulipa kodi na kuajiri watu. Kwa mjasiriamali wa aina hii hatakuwa na muda tena wa kuanza kuwaza yale yaliyotokea bali atakuwa anaiona dunia yenye matumaini kesho yake.
Atakuwa anafikiria zaidi juu ya siku za baadaye. Atakuwa na malengo ya kuhakikisha anaibadili dunia na wala siyo kusubiri dunia imbadilishe. Ni kwa sababu, akisubiri dunia imbadili, atakuwa miongoni mwa watu wanaosubiri kutupwa kwenye shimo la sahau.
Hii ina maana kuwa, mjasiriamali hatakiwi kukumbuka changamoto za jana kwa lengo la kumpa huzuni na machungu yatakayomsababisha ashindwe kupiga hatua. Bali anatakiwa kuchukulia changamoto hizo kama somo, ambalo litamwezesha kufika anakoelekea pasipo kurudi katika hali yake ya jana, ambayo siyo taswira nzuri katika kichwa chake.
Kama nilivyowahi kusema katika makala zangu za mwaka jana, mwanzo ni mgumu. Leo narudia tena kusema kuwa mwanzo ni mgumu. Mwanzo wa shughuli za ujasiriamali, wakati mwingine utaona kama hakuna anayekujali.
Unaweza kuhangaika siku nzima na hata zaidi ya miezi kadhaa pasipo kupata kile ulichokusudia. Wakati mwingine unaweza kuwa unatafuta msaada fulani ili kukamilisha kile ulichokianzisha ukaambulia patupu! Unaweza kuchekwa na baadhi ya watu, wakiwamo wale uliowategemea kuwa wangekuunga mkono. Pia, unaweza kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wajasiriamali wenzako, hata kwa wivu wake kana kwamba unapigana vita.
Hata hivyo, ukiamua kuona mbele utavuka vikwazo hivi vyote na kupata kile ulichokusudia. Kuona mbele ni pamoja na kuwa na dira au mweleko wa wapi unataka kuwa. Mjasiriamali mwenye dira huwa hakati tamaa na haogopi vita kutoka kwa wenzake au kwa baadhi ya watu. Ni mtu mwenye kuangalia ni njia zipi azitumie kufika pale anapotaka kufika.
Ikumbukwe kuwa ushindi huja kwa mtu mwenye kupambana kwa malengo ya kuiona kesho yenye nuru ya mafanikio.
Ushindi hupatikana na kujifunza kila hatua na njia anayoipita mjasiriamali ili kufika kwa mafanikio pale anapopata. Ili kufanikisha hili, mbali ya kuwa na maono, mjasiriamali anatakiwa kuwa mvumilivu na mwenye kuthubutu.
Uvumilivu na uthubutu ni miongoni mwa vitu muhimu sana kwa mjasiriamali. Ni vitu vinavyochangia suala zima la utekelezaji wa dira ya mjasiriamali, ambayo siku zote huwa ni kuona mbele. Kwa hiyo utakuja kutambua kuwa uvumilivu na uthubutu ndiyo silaha ya mjasiriamali kufikia kwenye mafanikio.
Watu wengi wameshindwa kufika popote kwa sababu ya kukosa uthubutu na uvumilivu wa kufanya yale wanayofikiria.
Kwa mjasiriamali anayethubutu na kuvumilia, ataiona kesho yake yenye neema na ambayo itamfaidisha yeye, jamii yake na Taifa kwa ujumla kwani mwendapole hajikwai, akijikwaa hataanguka wala kushindwa kuendelea na safari yake.
Makala hii imeandikwa na Chiraka Muhura wa Gazeti la Mwanachi.