Ni Ipi Imani Yako Kuhusu Mipango Uliyonayo?
Wednesday, December 22, 2021
Watu waliowengi ni kawaida kusikia wakisema jipe IMANI Mungu atakusaidia ufanikiwe au bora imani tu! utafanikiwa.
Pengine hali hii inatokana na msukumo ambao wamekuwa wakiupata kutoka kwa viongozi wa dini, ambao mara zote wamesisitiza waumini wao kuwa na IMANI; lakini..pasipo kuwambia, ni jinsi gani ya kuwa na hiyo IMANI.
Huwezi kuwa na IMANI hivihivi kutokea hewani tu! ni lazima IMANI yako ijengeke kutoka kwenye msingi fulani.
Kwa mfano msingi wa IMANI juu ya kupata PESA au MAFANIKIO ni kuanza KUTAMANI kitu fulani, halafu unapanga MPANGO wa jinsi ya kupata hicho kitu unachokitamani.
Kutokana na MPANGO, utatengeneza mchakato wa utekelezaji (mpango kazi) na hapa utatambua majukumu yako ya kufanya kila siku.
MPANGO ambao umejiwekea utaratibu wa kuupitia kila siku, utakujengea IMANI kwamba siku moja utafanikiwa kupata hicho unachotamani, kwasababu mpango utakuonyesha njia inayokwenda kufikia kile unachokitaka.
IMANI yako iliyojengwa katika msingi huu, inakufanya uweze kuwapuuza wakatisha tamaa wote ambao wamejaa sana mitaani kwetu.
Kwa hiyo, tunajifunza kwamba ni lazima tupange MIPANGO ya kupata PESA au kile tunachotamani kuwanacho. Japokuwa kuna imani kwamba mipango yote inapangwa na MUNGU, hivyo wasiojua ukweli huu hawaoni haja ya kupanga MIPANGO. Watu wengi wanadai kwamba wao wanaishi kwa IMANI na wanaichukulia siku kama ilivyokuja. Hii inamaanisha kwamba watu hawa huwa hawapangi siku yao, mwezi na hata mwaka.
Mungu wetu amekwishatupatia akili ya kutambua baya na zuri na pia tumepewa zawadi ya uwezo wa kupiga picha ya akili, ili kusudi tuweze kushiriki kwenye mchakato wa uumbaji na kutengeneza vitu mbalimbali kupitia MIPANGO.
Kwa kifupi ni kwamba, unahitaji MPANGO kuamini katika IMANI na ukweli ni kwamba:
“yeyote asiyekuwa na MPANGO wa kupata pesa hana IMANI ya kupata PESA”.
Unahitaji Mpango kazi wa kuamini kuwa utapata siku moja kile unachotamani kukipata. Kumbuka kuwa IMANI ya kweli inayojionyesha katika vitu viwili; yaani MPANGO na MATARAJIO.
IMANI siku zote, inatanguliwa na mawazo ya kitu Fulani (KUTAMANI), na baadae MPANGO KAZI (utekelezaji), ambao unakufanya upate kutambua majukumu ya kutimiza kila siku.
Utekelezaji wa majukumu yako ya kila siku unakupa MATARAJIO ya kufanikiwa. Matarajio ndiyo yanakujengea IMANI ya kwamba utafanikiwa siku moja.
Kwahiyo, MPANGO kwa maandishi juu ya kupata PESA au mafanikio yoyote, ndiyo inaonyesha matendo makuu ya kwamba UNAAMINI utapata pesa au mafanikio.