Watu Watano Hatari Ambao Hutakiwi Kufanya Nao Biashara.

Ili uweze kufanikiwa katika biashara unayoifanya ni muhimu kufanya biashara na watu sahihi ambao wanaweza kukusaidia hata wewe kuweza kusonga mbele. Watu hawa wanaweza wakawa ni wateja wako ama timu nzima inayokuzunguka na kukusaidia kukua katika biashara yako unayoifanya.
Inapotokea ukajikuta ukawa na ‘timu’ au watu unayofanya nayo biashara ikawa siyo sahihi sana kwako hapo ndipo matatizo na kushindwa mara nyingi huweza kuanza kujitokeza. Watu hawa ndiyo ambao tutawajadili katika makala hii, wale wanaoweza kutukwamisha na kutufanya tushindwe kufikia ndoto zetu tulizojiwekea.
Ni watu ambao tunawajua na tunashirikiana nao mara kwa mara katika shughuli tunazozifanya kila wakati za kibiashara. Kitu cha msingi na cha kujiuliza ni watu gani hasa ambao unatakiwa kuwaepuka na ambao wanaweza wakawa ni hatari kwa maendeleo ya biashara yako leo na kesho?
Hawa Ndiyo Watu Watano Hatari Ambao Hutakiwi Kufanya Nao Biashara.
1. Watu wanaokubali kila kitu.
Hawa ni watu ambao kila kitu wanachoambiwa huwa ni wepesi wa kukubali. Mara nyingi ni watu ambao hawana misimamo na wakati wowote wanaweza kuyumbishwa. Unapokuwa na watu kama hawa katika timu yako ya biashara inakuwa ni rahisi hata kwako wewe kuweza kukuangusha wakati wowote bila kutegemea.
Inapotokea kidogo tu wakapewa ushawishi na mtu mwingine pia ni rahisi kwao kuweza kukubali kwa sababu hiyo ndiyo asili yao. Kama unataka kufanya kazi au biashara yako vizuri ikafanikiwa zaidi, hakikisha unafanya kazi na watu wenye misimamo imara ambayo haiyumbishwi hovyo. Ikiwa utafanya kazi na watu hawa ‘Yes Man’ ipo siku watakukwamisha tu.

SOMA; Sababu 10 Zinazofanya Biashara Nyingi Mpya Zishindwe Kuendelea.



 2. Watu wanaochochea maneno.
Ni mara nyingi sana hawa ni watu ambao huwa tunao katika kazi zetu na pengine katika timu zetu za biashara. Hawa ni watu ambao mara nyingi hujifanya ni watu wa kupeleka sana habari kwa bosi wakati mwingine habari hizo wanazozipeleka zinaweza kuwa hata siyo za kweli kwa namna moja au nyingine ilimradi tu wazifikishe.
Unapokuwa na watu wa namna hii hata kama ni wawili katika bishara yako hicho ni kitu cha hatari kwako. Watu hawa wanakuwa wanauwezo mkubwa wa kuweza kuiharibu ama kuibomoa ‘Staff’ yako kwa jinsi wanavyoweza. Watu hawa wakati mwingine hufahamika kama wambea ambao kila mara hutaka kujifanya wako karibu na bosi, hivyo ni muhimu kuwaepuka sana katika kazi zetu na biashara kwa ujumla.
3. Watu wanaojua kila kitu.
Ni watu ambao huwa hawapo tayari kuelekezwa kitu kutokana na wao kujifanya wanajua kila kitu. Kama katika biashara yako una watu wa namna hii iwe wateja au wafanyakazi wako ama wafanyakazi wenzako hii itakupa tabu na shida kubwa sana katika suala zima la utendaji wa kazi.
Kwa maana kila utakachotaka kumwambia mtu wa namna hii, hata kama kuna sehemu amekosea utashindwa kwa sababu yeye anajua kila kila kitu. Najua bila shaka kwa namna moja au nyingine umewahi kukutana na watu wa namna hii katika eneo ulipo na unajua vizuri usumbufu wa watu hawa kuwa ni mkubwa.

SOMA; Mambo 12 Ya Kuzingatia Kama Unataka Kujiajiri.

 4. Watu wanaobadilika badilika.
Katika biashara yoyote unayoifanya, moja ya watu hatari wa kuwaepuka ni watu hawa wanaobadilika badilika kila wakati. Watu hawa mara nyingi huweza kubadilika zaidi kutokana na mambo mengi waliyonayo ndani mwao. Kitu kimojawapo kinachoweza kuwapelekea wao kubadilika zaidi ni tamaa walizonazo na kutokuwa waaminifu.
Unapoamua kufanya biashara na watu wa namna hii inakuwa siyo rahisi kwako kuweza kufanikiwa. Hii ni kwa sababu dakika na muda wowote ule ni rahisi sana kwao kuweza kukugeuka na inakuwa ni rahisi kuweza kukupa hasara ambayo hukutegemea. Dawa pekee ya kuweza kukwepa matatizo hayo ni kuwaepuka watu hawa kwa namna yoyote ile unayoweza.
5. Watu wanaolalamika sana.
Unapokuwa unafanya biashara na watu wa namna hii watakufanya ujihisi au uone kuwa wewe unakosea katika kila kitu. Hawa ni watu wenye tabia ya kulalamikia mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na huduma, pengine kwa kuona kwao mbovu au wananyonywa kwa namna moja au nyingine lakini ilimradi tu walalamike.
Ni watu ambao kiuhalisia ukiwa nao pamoja katika eneo la biashara ni rahisi sana kuweza kukuvunja hata moyo. Upo wakati utafika ambao unaweza ukahisi kweli kwa wanayolalamikia inaweza ikawa ni kweli kumbe hakuna hata ukweli wa kitu hicho hata kidogo kama wao wanavyodai iko hivyo.
Kumbuka, kama nilivyosema mwanzo unapokuwa na watu hawa inakuwa ni vigumu kwako kuweza kufanikiwa katika eneo la biashara unallolifanyia hata ufanyaje. Lakini kwa kifupi, hao ndiyo watu ambao tunao katika maeneo yetu ya kazi na ni muhimu kuwaepuka ili kuweza kufanikiwa zaidi.
Tunakutakia kila la kheri, endelea kutembelea kujifunza na kuhamasika zaidi. Pia hakikisha unawashirikisha wengine waendelee kujifunza kupitia mtandao huu.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,


Iklan Atas Artikel

Iklan Tengah Artikel 1

Iklan Tengah Artikel 2

Iklan Bawah Artikel