Misingi 6 Muhimu Ya Kujiwekea, Ili Kujenga Mafanikio Ya Kudumu.

Ili uweze kufanikiwa, ni lazima kujiwekea misingi imara ya kimafanikio itakayokuwa ikukuongoza kila siku. Bila kuijua misingi hii mapema sitashangaa kuona maisha yako yakibaki kuwa yaleyale bila ya kubadilika sana. Kwa kujiwekea misingi hii, inauwezo wa kufanya maisha yako kubadilika kwa sehemu kubwa sana.
Kama misingi hiyo ipo, ni nini kinachokuzuia wewe kufanikiwa sasa? Bila shaka hakuna. Unachohitajika kukifanya ni kutumia misingi hiyo mpaka kufanikiwa. Uwezo na nguvu za kubadilisha maisha yako kwa kadri unavyotaka unao. Kwa kuijua misingi hii, kwako itakuwa chachu ya kukusaidia kuweza kusonga mbele na kujijengea maisha ya mafanikio makubwa:-
Je, misingi hiyo ni ipi?
Hii Ndiyo Misingi 6 Muhimu Ya Kujiwekea, Ili Kujenga Mafanikio Ya Kudumu.
1. Kaa mbali na watu hasi.
Kama vile ambavyo ilivyo kompyuta inaweza ikaharibiwa na virusi na kuharibika kabisa, hata wewe maisha yako yanaweza kuharibiwa vivyohivyo lakini ikiwa una watu hawa hasi wengi wanaokuzunguka. Unapokuwa na watu hasi inakuwa ni rahisi sana kwako kuweza kuua mipango na malengo mazuri uliyojiwekea.
Ninajua watu hawa wanaweza wakawa ni rafiki zako au ndugu kabisa, lakini hiyo haina namna tena kwako, zaidi ya kuachana nao. Ikiwa utaendelea kung’ang’ania kuwa na watu hawa hasi utarudishwa nyuma sana katika maisha yako. Ili kuokoa maisha yako ni lazima kukaa mbali nao na kutafuta marafiki chanya watakaokupa hamasa ya kufanikiwa zaidi. Kukaa mbali na watu hasi ni msingi mzuri kwako unaotakiwa kuujua.

2. Wekeza kila siku katika maisha yako.
Huu ni msingi muhimu sana kujiwekea ili kuwa na mafanikio ya viwango vya juu. Kama katika maisha yako unawekeza kila siku, tambua baada ya muda kidogo kuanzia sasa utakuwa mbali sana kimafanikio. Pengine unaweza ukaanza kusema ‘oooh mimi sasa sina pesa, sina mtaji hili halinihusu nitawekeza vipi sasa hapa?’
Sikiliza, hauhitaji kuwa na pesa ili kuwekeza. Anza na kuwekeza kwanza kwenye akili yako kwa kujifunza kupitia vitabu au semina mbalimbali. Maisha yako yatakuwa ya thamani sana kila utakavyozidi kufanya uwekezaji huu. Maarifa utakayoyapata huko kwani yataweza kukusaidia kuwekeza katika maeneo mengine na kufanikiwa zaidi pale utakapopata mtaji unaouhitaji.
3. Kuwa wewe kama wewe.
Kuna wakati wengi wetu huwa ni watu wa kutaka maisha ya kuwapendezesha wengine. Nikiwa na maana kutaka kuishi maisha kama wengine wanavyoishi. Hiki ni kitu hatari sana kwako kwa sababu unakuwa unaishi kwa kufuata bendera ama wengine wanavyoishi na kujikuta unakuwa mtu wa kupoteza mwelekeo.
Ili uweze kuishi kwa mafanikio ni vizuri ukajijengea msingi wa kuishi maisha yako ukiwa wewe kama wewe. Kwa kuishi wewe kama wewe itakulazimisha kutambua  unataka nini kwenye haya maisha, ni lini utafikia mipango yako uliyojiwekea na unataka kitu gani kikusaidie kufikia malengo yako. Huo ndiyo msingi muhimu pia kuujua kwa ajili ya mafanikio yako ya leo na kesho.
4. Jiwekee mipaka katika maisha yako.
Ishi maisha yako kwa kujiwekea mipaka. Usije ukaruhusu kila mtu kuingilia maisha yako kwa jinsi anavyotaka hata respeto ndugu wa karibu kiasi gani. Bila shaka umeshawahi kuona watu ambao maisha yao yanaharibiwa kutokana na kuingiliwa na watu walio karibu nao. Na hii yote imekuwa ikitokea kutokana na wahusika kushindwa kujiwekea mipaka iliyoimara katika maisha yao.
Mipaka hii unatakiwa ujiwekee katika maeneo mabalimbali kama vile katika muda, kazi zako za kawaida na wakati mwingine kwenye biashara zako unazozifanya. Kwa kufanya hivyo watu wako wa karibu watakuwa hawako huru sana kuingilia yale maeneo uliyojiwekea mipaka maana wakifanya hivyo watajua utakuwa mkali au hutakubali kiurahisi. Hiyo itakusaidia kukujengea msingi mwingine imara wa mafanikio yako.
5. Kuwa king’ang’anizi wa mafanikio.
Kwenye maisha yako kitu ambacho hutakiwi kukiruhusu ni kushindwa kiurahisi. Kama ikitokea umeshindwa katika jambo kwa namna  moja au nyingne, jaribu kutafuta njia ya kulifanya jambo hilo kwa namna ya tofauti mpaka kufanikiwa. Unapokuwa king’anga’nizi wa mafanikio huo utakuwa msingi bora kwako unaojitengenezea wa kufikia mafaniko makubwa.
Maisha ni kusonga mbele. Ng’ang’ania mafanikio yako mpaka uyaone hata kwa gharama yoyote ile. Usiruhusu kitu kikakukatisha tamaa. Kama unafikira za nyuma unazoziweza kwa kudhani kuwa ulikosea eneo fulani ni bora ukaachana nazo fikra hizo kwa sasa, kwa sababu hazitakusaidi kitu chochote zaidi ya kukwamisha wewe. Yaliyopita yamepita, songa mbele.
6. Jijengee ukomavu wa fikra.
Ili uweze kufanikiwa inatakiwa ifike mahali fikra zako ziwe zimekomaa na kuweza kutambua kila hali inayojitokeza katika maisha na jinsi ya kuweza kukabiliana nayo. Kwa mfano, inapotokea kushindwa au ukakosea katika jambo fulani unakabiliana vipi na kushindwa huko bila kuumia au kujiona hufai na kisha kuendelea mbele.
Hakuna kingine zaidi ya wewe kuwa na ukomavu fulani wa fikra utakao kuwezesha kusonga mbele. Ukomavu huu ni rahisi kuupata, utaupata tu ikiwa wewe ni mtu wa kujifunza mambo mbalimbali ya kimafanikio kama unavyofanya sasa hivi. Bila kufanya hivyo hutaweza kuhimili mawimbi mengi ya maisha yanayojitokeza kwa upande wako.
Kumbuka hii ni sehemu ya misingi ambayo unaweza ukajiwekea kama nguzo ya mafanikio yako. Lakini, kwa kutumia kijitabu chako kidogo cha kujifunzia unaweza ukaongeza misingi mingine ambayo unaona kwako inafaa kukuongoza katika safari ya mafanikio. Bila kujiwekea misingi binafsi, utayumbishwa sana katika maisha kwa mambo mengi na itakuwa ngumu kufanikiwa.
Tunakutakia kila la kheri katika safari ya mafanikio, endelea kuwashirikisha wengine kutembelea mtandao huu wa kila siku kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 80 35,




Iklan Atas Artikel

Iklan Tengah Artikel 1

Iklan Tengah Artikel 2

Iklan Bawah Artikel