Misingi Mitatu Ya Kuzingatia Unapoamua Kuweka Malengo.
Saturday, April 30, 2022
Ili uweze kufikia malengo yako, ipo misingi ya kuzingatia na kuifanyia kazi kila siku. Kama utashindwa kuifanyia kazi misingi hiyo, nikwambie kwako itakuwa ni kazi ngumu sana kuweza kufikia malengo yako uliyonayo.
Tunaona watu wengi wanakuwa na malengo, lakini watu hawa wanakuwa wanashindwa kuyafikia kwa sababu wanakuwa hawana misingi sahihi ya kuweza kuyafikia. Je, uko tayari kuijua misingi ya kufata ili kufikia malengo yako?
Kama ni ndio, karibu ujifunze misingi hiyo kupitia makala haya;-
1. Weka malengo yanayofikika.
Unapoamua kuweka malengo yako na ukawa na nia thabiti ya kuyafikia, unatakiwa kuhakikisha unajiwekea malengo ambayo unaweza kuyafikia. Usiweke malengo ilimradi tu, weka malengo ya wewe kuweza kuyafikia.
Hapa katika kufanikisha zoezi hili, usijaribu hata kidogo kuweka malengo makubwa sana na ambayo kwenye utekelezaji yatakukatisha tamaa. Weka malengo ambayo yako ndani ya uwezo wako na una uwezo ya kuyamudu kuyafikia.
2. Usijiwekee malengo mengi sana.
Kujiwekea malengo kwa wakati mmoja huko ni sawa na kujiandaa kushindwa. Weka malengo ambayo ni machache na utayafanya kwa uhakika, kuliko kuweka malengo ambayo ni mengi na inakuwa shida kwako kuyafikia.
Kwa mfano unaweza ukaweka malengo ya kusoma kitabu kimoja kila mwezi. Unaweza ukaweka lengo la kuboresha afya yako kila siku kwa kukimbia kidogo. Unapoweka lengo moja, hiyo inakupa hamasa na nguvu ya kuweza kutenda zaidi na zaidi.
3. Fanya marekebisho ya malengo yako inapohitajika.
Usiweke malengo tu na ukaamua kuyaacha kama yalivyo, jitahidi sana, kufanya marekebisho ya malengo yako kila wakati hasa pale inapohitajika. Kuweka malengo kwa kuyamiminia zege huko ni kujipoteza.
Ukizingatia mambo hayo matatu, utakuwa upo kwenye misingi sahihi wa kuweza kuyatimiza malengo yako au kuyafikia kabisa. Kitu kikubwa kwako ni kuamua kuchukua hatua za kila siku. Kumbuka, ufalme hauji kwa maneno bali unakuja kwa vitendo.
Nikutakie kila la kheri,
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA NDOTO ZAKO ZITUMIE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
Mawasiliano, Whats app; 0713048035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com