Dalili Tano (5) Zitakazokuonyesha Kwamba Upo Kwenye Njia Sahihi Ya Mafanikio Yako.
Tuesday, July 5, 2022
Kila mtu mwenye nia ya kutafuta mafanikio, kuna wakati anakuwa ana shaka kwamba je, ‘kweli nipo kwenye njia sahihi ya kufanikiwa au hapana.’ Hali hii hujitokeza kwa sababu, njia ya mafanikio inakuwa in changamoto nyingi sana.
Kuna wakati inafika kutokana na changamoto hizo, wengi huanza kukata tamaa na kuanza kujiuliza maswali kweli njia hiyo au hicho wakifanyacho kinawafikisha kwenye mafanikio yao, au kinawatoa nje kabisa ya mafanikio.
Hali kama hii inajitokeza kwa wengi sana si kwako tu, bali hata kwa watu waliofanikiwa ikiwemo pamoja na mamilionea hufika wakati wakijiuliza je, kwa kile wakifanyacho kwa wakati huo kinawafikisha kwenye mafanikio mengine ya juu zaidi au hapana.
Kitu cha kujiuliza zaidi, utajuaje kwamba upo kwenye njia sahihi ya mafanikio yako? Hiki ndicho kitu ambacho nataka ujifunze kupitia makala haya ili tena usiwe na shaka. Kama utakosa dalili hizo kabisa miongoni mwa hizi ujue upo nje ya mafanikio.
Zifuatazo Dalili Tano (5) Zitakazokuonyesha Kwamba Upo Kwenye Njia Sahihi Ya Mafanikio.;-
1. Kama wewe ni king’ang’anizi.
Mafanikio kila wakati yanawapendelea na kwenda kwa watu ambao ni ving’ang’anizi na ambao wana nidhamu ya kujua kile wakitakacho na kukifanya kwa muda mrefu. Hakuna mafanikio yanayokwenda kwa mtu ambaye si king’ang’anizi.
Mfumo na njia unayoipitia ya ung’anganizi ndio inayotabiri kwamba wewe unakwenda kufanikiwa. Nafasi yako ya kufanikiwa itakuwa kubwa sana kama ni king’ang’anizi, tofauti na yule ambaye si king’ang’anizi kwani mtu huyo lazima atashindwa.
Ukishajua kile unachokitaka vizuri, ni vyema ukawa king’ang’anizi kwani ni dalili tosha ya kwamba kitu hicho ukitakacho utakipata. Ukikosa ung’ang’anizi, ujue kabisa hautaweza kufanikiwa hata kama ungeweka juhudi kubwa sana.
2. Kama una mahusiano sahihi na pesa.
Mahusiano hayaishii tu kwa watu lakini pia ili kufanikiwa, unatakiwa kuwa na mahusiano sahihi na pesa. Si kwa sababu unapata pesa ukaamua kuzitumia pesa hizo hovyo hovyo na kufanya vitu vya ‘biashara kichaa’ ambazo hata hazieleweki.
Mahusiano sahihi yanakuja kwa wewe kutuliza akili yako, kwa kila pesa unayoipata kuiwekea akiba hata kama ni kidogo sana, kuwekeza kwa busara na mengine kama haya. Unapokuwa hauna mahusiano sahihi na pesa, huwezi kufanikiwa.
Unatakiwa ujikague na kujitathimini, je unayo mahusiano sahihi na pesa. Kila unapoangalia matumizi yako, je, yamekaa sawa? Kama ukiona una mahusiano sahihi na pesa, basi ujue upo kwenye njia sahihi ya kuweza kufikia mafanikio yako.
3. Kama una mahusiano sahihi na watu sahihi.
Kupata mafanikio kunategemea mambo mengi sana, ikiwemo mojawapo la msingi sana ni kuwa na watu sahihi. Kuwa na mahusiano na watu sahihi ni kitu cha muhimu sana katika kukupa mafanikio uyatakayo maishani mwako.
Watu sahihi wanakuwa wanakupa chachu na hamasa kubwa ya kukupeleka mbele kimafanikio. Unapowakosa watu hao unakuwa unatoka nje ya mafanikio yako na mwisho wa siku utashangaa umeshindwa vibaya sana.
Jiangalie wewe mwenyewe na ujiulize je, una timu sahihi inayokuzunguka ya watu ambao watakusaidia kukupa mafanikio yako? Kama huna timu hiyo itafute, kwani dalili mojawapo inayoonyesha kwamba utafanikiwa ni watu sahihi ulionao.
4. Kama unajua mapema kile kinachofanya kazi.
Watu wenye mafanikio wanajua mapema sana yale mambo yayofanya kazi kwao na yale ambayo hayafanya kazi. Kama kuna jambo wanalifanya, wakigundua jambo hilo linawapeleka eneo ambalo si sahihi hukimbia sana na kutafuta kitu kingine.
Kile kitakachokufanya ujijue pia uko kwenye njia sahihi ya kutafuta mafanikio yako ni kule kuwa makini na kujua kile unachokifanya kama kinafanya kazi yaani kinaleta matunda ambayo unayataka na kwa muda mwafaka unaoutaka wewe.
Ni jukumu lako kukagua kile unachokifanya na kujiuliza maswali ya msingi, je, hiki nikifanyacho kinafanya kazi au hakifanya kazi, kujiuliza maswali haya itakusaidia sana kujua njia ya mafanikio unayopita ipo sahihi au haipo sahihi.
5. Kama una imani ya kufikia mafanikio yako.
Imani ni moja ya kitu kikubwa sana ambacho kinaweza kikakufikisha kule kwenye mafanikio yako. Kila unapofikiria ndoto yako kama una imani kuna kitu ambacho unajiambia ni lazima nitafanikisha hili au ni lazima nitafanya jambo lile.
Ile imani unayojiambia wakati unatafuta mafanikio, hiyo ndio imani unayatakiwa kuwa nayo. Imani hii ya kuweza haiji kwa bahati mbaya, bali inakuja pale unapokuwa na mipango imara na kutambua jinsi unavyoweza kufikia ndoto zako.
Nikuulize hapo ulipo una imani ya kuamini kwamba utafikia ndoto zako. Imani hii hata kama huna, unatakiwa ujue jinsi ya kuweza kuimiliki ili ikusaidia kufika kule unakotaka kufika. Mafanikio yako yanahitaji sana uwe na imani hii ya msingi.
Kwa maelezo haya yakinifu, hizi ndizo dalili za msingi za kujua kama upo kwenye njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio. Fanyia kazi hiki ulichojifunza na chukua hatua mathubuti zitakazoweza kukusaidia kufikia ndoto zako.
Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza maisha na mafanikio.
Pia rafiki, kama unapenda kujifunza zaidi kuhusu mafanikio, karibu kwenye kundi la WHATS APP LA MAFANIKIO, kujiunga tuma neno THE UNIVERSITY OF WINNER’S kwenda 0713 048 035, hapo utapata utaratibu mzima wa kujiunga.
Kama wewe ni mfugaji wa kuku na unahitaji vifaranga bora, waone DM POULTRY FARM PROJECT kwa huduma ya uhakika. Hawa ni wauzaji wa vifaranga wa kuku aina ya KUROILER, SASSO, KIENYEJI ASILIA na KUCHI. Kwa mahitaji ya vifaranga wasiliana nao kwa 0767 048 035 au 0686 141097 na wote mnakaribishwa.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com